Kundi la wachunguzi wa kimataifa waliochunguza kutunguliwa kwa ndege ya shirika la Malaysia Airlines safari nambari MH17 mashariki mwa Ukraine mwaka 2014 wamesema kombora lililotungua ndege hiyo lilirushwa kutoka maeneo yaliyodhibitiwa na waasi walioungwa mkono na Urusi.
Kundi hilo, likitoa ripoti yake ya awali ya uchunguzi nchini Uholanzi, limesema kombora lilirushwa kutoka karibu na kijiji cha Pervomaiskiy.
Wachunguzi hao pia wamesema kombora hilo aina ya BUK lililoundiwa nchini Urusi pamoja na mtambo wa kurusha kombora hilo, vilitolewa Urusi na vilirejeshwa huko siku iliyofuata.
Wachunguzi hao, ambao wamekuwa wakikusanya ushahidi kwa lengo la kubaini uwezekano wa kufunguliwa kwa kesi ya jinai, wanasema wanachunguza watu karibu mia moja waliohusishwa na shambulio hilo ingawa si kwamba wote ni wachunguzi.
Kundi hilo la wachunguzi wa kimataifa liliongozwa na wataalamu kutoka Uholanzi, wakishirikiana na wataalamu wa mashtaka kutoka Australia, Ubelgiji, Malaysia na Ukraine.
Watu wote 298 waliokuwa kwenye ndege hiyo aina ya Boeing 777 iliyokuwa safarini kutoka Amsterdam kuelekea Kuala Lumpur walifariki baada ya ndege hiyo kuanguka eneo la Grabovo jimbo la Donetsk .
Uchunguzi wa awali ulioongozwa na Bodi ya Usalama ya Uholanzi ulisema kombora aina ya Buk lililoundiwa Urusi lilitumiwa kutungua ndege hiyo.
Nani wa kulaumiwa?
Waasi walioungwa mkono na Urusi walilaumiwa na Ukraine na nchi za Magharibi na kudaiwa kutungua ndege hiyo 17 Julai 2014.
Wakati huo, wanajeshi wa Ukraine walikuwa kwenye vita vikali na waasi hao waliotaka kujitenga kwa maeneo ya mashariki mwa Ukraine.
Urusi imekana kuhusika na pia kupuuzilia mbali madai kwamba mtambo uliorusha kombora hilo la Buk ulikuwa maeneo ya Urusi.
Lakini baada ya kisa hicho, Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani waliiwekea vikwazo Urusi.
Mapema wiki hii, Urusi ilitoa picha za mitambo ya rada, ambazo ilisema zinaonesha ndege hiyo haingetunguliwa na watu kutoka maeneo yaliyoshikiliwa na waasi.
Wakosoaji wa Urusi wanasema Urusi imetoa simulizi tatu tofauti kuhusu matukio yaliyojiri wakati wa kutunguliwa kwa ndege hiyo.
SORCE : BBC
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni