.

Jumamosi, 23 Julai 2016

Koffi Olomide akamatwa na kuzuiliwa Nairobi


Mwanamuziki mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Koffi Olomide amekamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa polisi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Olomide amekamatwa muda mfupi baada ya kumaliza mahojiano katika kituo kimoja cha runinga jijini Nairobi.

Mkuu wa polisi nchini Kenya Joseph Boinnet alikuwa ametoa taarifa na kuwaagiza polisi wachukue hatua.

Mwanamuziki huyo alikuwa amekabiliwa na shutuma baada ya kanda ya video kuenea mtandaoni ikionekana kumuonyesha akimshambulia mwanamke uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta Ijumaa asubuhi, muda mfupi baada ya kuwasili.
Mwanamke huyo anadaiwa kuwa mmoja wa wachezaji ngoma wake.

Akiongea katika kituo cha televisheni ya Citizen, muda mfupi kabla ya kukamatwa, Olomide alijitetea na kusema hakukusudia kumshambulia mwanamke huyo.

Alisema alikuwa ameingilia kisa ambacho aliamini ni mtu aliyetaka kumpokonya mmoja wa wachezaji densi wake pochi yake au kulikuwa na vurugu fulani.

Awali, kwenye ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook, alisema tukio hilo lilieleweka vibaya.

Alisema alikuwa anajaribu kumtetea mwanamke huyo kwani mmoja wa maafisa wa kike katika uwanja huo wa ndege alikuwa akiwasumbua wasichana hao wachezaji ngoma aliokuwa wakiandamana naye.

Katika video hiyo msichana huyo mchezaji anaonekana kukubaliana naye.

Mwanamuziki huyo, alikuwa amepangiwa kutumbuiza mashabiki katika ukumbi wa Bomas siku ya Jumamosi.

Baada ya kuenea kwa habari kuhusu kisa hicho cha uwanja wa ndege, wengi wa Wakenya wamemshutumu na kutoa wito kwao watu kutohudhuria tamasha hilo na badala yake wakitaka akamatwe.

Wengine kupitia kitambulisha mada #KickKoffiOlomideBackToCongo kwenye Twitter wakipendekeza afurushwe kutoka Kenya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni