.

Jumamosi, 8 Oktoba 2016

Chris Brown apatawa na kashfa Kenya

Muimbaji mashuhuri wa Marekani mtindo wa Hip Hop Chris Brown, yupo Kenya kwa tamasha la muziki mjini Mombasa eneo la pwani.
Lakini tukio ambalo halikunukuliwa kwenye kamera limegubika vyombo vya habari nchini.
Shabiki mmoja mwanamke anatuhumu kuwa Chris Brown ameivunja simu yake alipojaribu kupiga picha 'selfie' alipowasili katika uwanja wa ndege Mombasa.
Kwa mujibu wa gazeti mmoja nchini "Daily Nation,'' mwanamke huyo anasema CB alimpokonya simu kutoka nyuma alipojitayarisha kuipiga picha hiyo na kuirusha chini.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa simu ya msichana huyo aina ya iPhone 6 iliyomgharimu takriban dola 900, haikuvunjika lakini kizuia kioo na kifunikio cha simu viliharibiwa.
Shabiki huyo aliyesema amenunua tiketi kuhudhuria tamasha hilo, ameghadhabishwa na ameamua kutohudhuria tamasha hilo.
Tuhuma zake zimesababisha gumzo kuu katika mtandao wa Twitter kupitia #DeportChrisBrown ambapo Wakenya wanajadili iwapo muimbaji huyo nyota arudishwe Marekani.
Hisia zimegawanyika ambapo baadhi wanamtetea Chris Brown na wengine wakitaka atimuliwe Kenya.
Kanda ya video iliyowekwa na @KinyanBoy katika twitter inaonekana kumuonyesha Chris Brown akipuuza ombi la mwanamke huyo kupiga selfie na anampita bila kumgusa.
Lakini mwanamke huyo aliyejitambulisha kama Brenda Chepkoech, amezungumza na televisheni ya NTV nchini, anasisitiza kuwa tukio hilo limetokea baada ya kanda hiyo kuwekwa kwenye mtandao na ni muda mfupi kabla ya CB kuingia garini na kuondoka.
Mnamo Julai mwanamuziki mashuhuri wa Congo, Koffi Olomide alirudishwa Congo kutoka Kenya baada ya kuzuka video katika mitandao ya kijamii akionekana kumpiga teke mojawapo ya wachezaji wake densi katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta Nairobi.
Wakenya walighadhabishwa katika Twitter na kutaka atimuliwe.
Koffi aliomba radhi lakini tamasha lake lilifutiliwa mbali na alirudishwa Kinshasa kwa ndege.
Siku chache baadaye waandalizi wa tamasha lake jingine Zambia pia walilazimika kufutilia mbali tamasha hilo kutokana na shinikizo kufuatia tukio la Kenya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni