Donald Trump ni tajiri anayemiliki majumba mengi na ambaye amekuwa mtangazaji wa kipindi cha maisha ya uhalisia kwenye runinga.
Amekuwa mtu anayeangazia sana ushindi katika maisha yake na anasema ni lazima afanikiwe katika kupata tuzo kuu duniani, kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Tayari ameidhinishwa na chama cha Republican kuwania urais baada ya kuwabwaga wapinzani wengine.
Kwa wafuasi wake, mgombea huyu wa Urais kwa chama cha Republican ndiye anayeweza kuleta ufanisi kwa Marekani.
Kwao, huyu ni tajiri shupavu anayeweza kusuluhisha matatizo yote ya nchi ambayo wanahisi yameshusha hadhi ya Marekani duniani.
Wengi wao ni raia wa Marekani wafanyikazi hasa wenye asili ya Kizungu na walio na maisha ya kadri.
Mbaguzi na mfitini
Hata hivyo kwa wakosoaji wake, wanasema huyu ni mbaguzi na mfitini, muonevu mkubwa ambaye atapokeza ushindi kwa Hillary Clinton au kuitumbukiza dunia kwenye janga kubwa.
Sasa ndoto ya kisiasa ya BwTrump inakaribia kutimia, hasa baada ya kushinda mchujo wa chama cha Republican, kinyume na matarajiyo ya wengi.
Ni ushindi ambao umetajwa kuwa wa kihistoria katika siasa za Marekani.
Trump ameamua kuvunja desturi ya siasa za Marekani.
Anawatusi wanawake, raia wa Mexico, Waislamu na yeyote yule anayemkera wakiwemo wapinzani wake 16 aliokabiliana nao katika mchujo wa Republican.
Alimdharau Jeb Bush na kumueleza kama mtu asiye na nguvu yeyote, akamdunisha Rubio kama Kitoto na akaelekeza makali yake kwa Cruz akimuita mrongo.
Kauli zake kali Bw Trump pamoja na chuki aliyonayo dhidi ya utawala imeonekana kuwavutia wengi.
Ameahidi kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico, kuwarejesha kwa nguvu mamilioni ya wahamiaji haramu, pamoja na kuzima Uchina, ili muradi kuhakikisha Marekani inarejesha nguvu zake tena katika dunia.
Kusafiri kwa Boeing 757
Mwanasiasa huyu husafiri kwa ndege ya binafsi aina ya Boeing 757 kwenye mikutano yake ya kampeni. Huvutia umati wa watu na waandishi habari sawa na nyota wa mziki.
Yeye aliongoza katika kuangaziwa katika taarifa za runinga kuwaliko wapinzani wake wote kwa pamoja katika mchujo wa Republican.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, taarifa za Trump kwenye runinga zilileta dola bilioni mbili, bila yeye kugharamia.
Mwanzo wa kampeni hizi, swali kubwa lilikia ikiwa kura za maoni zilizomueka Trump kifua mbele zingemuwezesha kuzoa kura halisi?
Baada ya kushindwa mchujo wa kwanza na Ted Cruz katika jimbo la Iowa, Trump alijikwamua na aliendeleza ushindi ambao haungeweza kuzimwa ambapo aliwapiku wapinzani wake katika majimbo ya kwanza ya New Hampshire na South Carolina.
Aidha Jumanne Kuu ya tarehe 1 mwezi wa Machi, alizoa ushindi katika majimbo saba kati ya 12 ambako mchujo ulifanyika.
Mwisho alishinda katika majimbo saba zaidi ikiwemo Indiana.
Sasa swali kubwa hapa ni iwapo Trump atafanikiwa katika kura ya urais hapo mwezi Novemba.
Wazazi wa Trump
Donald Trump alizaliwa Juni 14 mwaka wa 1946, mjini New York, akiwa mtoto wa tano kati ya watoto sita.
Babake Fred alikuwa tajiri aliyemilki majumba na babu zake Trump walikua wahamiaji kutoka Ujerumani.
Mamake Mary alikua mzaliwa wa Scotland.
Tangu utotoni, Trump alikuwa mtundu na wazazi wake walimpeleka shule ya msingi iliyofadhiliwa na jeshi mjini New York.
Baadaye alifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania, kitivo cha elimu ya biashara mwaka wa 1968.
Alifanya kazi katika kampuni ya babake ambaye aliendesha biashara ya kuuza nyumba kwa raia wa kipato cha kadiri, viungani mwa New York.
Hata hivyo Donald Trump alikuwa na ndoto ya kufanya biashara nje ya makaazi ya Queens na Brooklyn.
Aliwekeza katika biashara kubwa ya ujenzi na kuweza kujenga mojawapo ya mijengo ya kifahari zaidi nchini Marekani.
Alifanikiwa kutokana na sera ya kiuchumi iliyowekwa na utawala wa Reagan miaka wa 1980.
Kuna tofauti kuhusu utajiri hasa wa Trump.
Aliwahi kuambia tume ya uchaguzi kwamba anao utajiri wa kima cha dola bilioni 10.
Hata hivyo jarida la Forbes limenadi kwamba utajiri wa Trump haufikii juu ya dola bilioni 4.5.
Lakini unapotembea barabara kuu za Manhattan, kampuni ya Trump imeweka mabawa yake kwa majumba ya kifahari yaliyofuatana.
Yapo mahoteli, viwanja vya mchezo wa gofu, makazi ya kifahari, majumba ya kamari kutoka Carlifonia hadi Mumbai nembo yake ikiwa ni Trump.
Ameandika Riwaya kadhaa kuhusu biashara, huku umaarufu wake uking'aa zaidi katika makala yanayoelezea maisha halisi, "The Apprentice," katika runinga ya NBC. Hata hivyo alitupwa nje ya makala hayo baada ya kutoa kauli zilizowakera raia wa Mexico.
Matusi
Licha ya kufanikiwa katika biashara, Trump pia amefeli kwenye hizo biashara na maisha. Kwa mara nne kati ya mwaka 1991 na 2009, miradi yake ya hoteli na majumba ya kamari ilitangazwa kufilisika.
Ndoa zake tatu zimevunjika, pia alikejeliwa kwenye vyombo vya habari kwa kudai kwamba cheti cha kuzaliwa cha Rais Barack Obama hakikua cha Marekani.
Wengi walimcheka alipotangaza nia yake kuwania urais wa Marekani.
Haijalishi matusi anayotoa, wafuasi wake wameendelea kusimama naye na kumpenda zaidi.
Aliwaita wahamiaji kutoka Mexico kama wabakaji, na kusema mtangazaji wa runinga ya Fox alimuuliza maswali magumu kwa sababu alikuwa anapata hedhi.
Alivutia lalama za kimataifa baada ya kusema ataweka marufuku kwa Waislamu wote kuingia Marekani kwa muda.
Saa kadhaa kabla ya kushinda mchujo wa jimbo la Indiana, na kumshinda Cruz, alitoa madai kwamba babake Cruz alihusishwa na mtu aliyemuua Rais John F. Kennedy.
Licha ya haya yote, watu wengi wameendelea kuvutiwa na mwanasiasa huyu ambaye amesema ataweka ujuzi na mafanikio yake binafsi kuboresha hadhi ya nchi.
Aliwahi kuwa mwanachama wa Democratic, na pia akajiunga na upande wa kujitegemea.
Trump sasa amebadilisha msimamo wake wa kadri kuhusu umiliki wa silaha, utoaji wa mimba na kutetea msimamo mkali huku akiwapuuza wanachama wa Republican walio na msimamo wa kadiri.
SOURCE:BBC
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni