KAMPUNI ya Ndege ya Tanzania (ATCL), imeanzisha safari za kutoka Tabora kwenda mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam ikiwa na lengo la kurahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa mikoa hiyo na ile ya jirani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alisema katika uzinduzi wa huduma hiyo kuwa kuanzishwa kwa safari hizo kutaongeza wigo wa biashara na kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo utalii na kilimo.
“Naamini wakazi wa mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani, sasa mtanufaika kwa ujio wa ndege hii, matumaini yangu kwamba mtatumia usafiri huu kurahisisha shughuli zenu za kibiashara na kijamii,”alisema.
Ngonyani aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kutumia fursa ya ujio wa ndege hiyo kama chachu ya kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Sambamba na hilo, Ngonyani alisema katika kuhakikisha usafiri wa anga unaimarika nchini, Serikali itaongeza ndege nyingine tatu katika mwaka wa fedha 2017/18 ambapo hadi kufikia mwezi Julai mwakani ndege hizo zitakuwa zimewasili.
Katika hatua nyingine, Ngonyani amewaagiza wafanyakazi wa ATCL kufanya kazi kwa juhudi, uadilifu na weledi ili kuijengea sifa kampuni hiyo na kuvutia wateja ili kujiimarisha katika soko la ushindani.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Sekta ya Uchukuzi), Dk. Leonard Chamuriho aliwataka wananchi wa mkoa huo kutumia fursa ya kupata usafiri wenye gharama nafuu na wa muda mfupi.
Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri aliwataka wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutumia huduma za usafiri huo waliokuwa wakiusubiri muda mrefu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni