Rais John Pombe Magufuli
Kwa ufupi
Hatimaye mjane aliyemwaga machozi mbele ya Rais John Magufuli amepewa nyumba na shamba baada ya Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Crispin Meela kusuluhisha mgogoro wa umiliki wa mali hizo.
Babati. Hatimaye mjane aliyemwaga machozi mbele ya Rais John Magufuli amepewa nyumba na shamba baada ya Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Crispin Meela kusuluhisha mgogoro wa umiliki wa mali hizo.
Hivi karibuni akiwa mjini Babati, Rais Magufuli alimuagiza Meela ahakikishe mjane huyo, Mwanaidi Mussa anapewa mali zake ikiwamo nyumba na shamba anazodai kuwa mke mdogo amemdhulumu baada ya mume wao kufariki dunia.
Meela alimkabidhi mjane huyo juzi nyumba na shamba la ekari 2.5 iliyokuwa inagombaniwa na mke mdogo na kuagiza endapo hakuridhika na uamuzi huo akate rufaa katika mahakama ya juu na siyo kuamua mambo bila kufata sheria.
Meela pia amewataka wananchi kuacha kurubuniwa na watu wachache wenye maslahi binafsi na badala yake wafuate maelekezo kutoka katika vyombo vya dola na sio kufuata ushabiki katika migogoro yao pindi inapotokea.
“Migogoro ya mirathi imeendelea kukithiri katika maeneo mengi nchini kutokana na watu kutofuata sheria za mirathi na wengine wakitaka kunufaika na mali zinazoachwa na marehemu," alisema Meela.
Mwanaid ambaye kwa sasa ni mtu mzima alisema kwa muda mrefu amewaomba viongozi wa serikali ya mtaa anaoishi wamsaidie lakini wameshindwa kumsikiliza na badala yake wanaegemea upande mmoja jambo lililozidisha mgogoro huo.
Mkwa upande wake mke mdogo, Asia Musa alisema kuwa nyumba hiyo alijenga yeye na mume wake kabla hajafariki ambapo kauli yake ilikinzana na mke mkubwa aliyesema kuwa mke mdogo alikuta nyumba hiyo imeshajengwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni