.

Jumanne, 10 Mei 2016

Jinsi ya kuanzisha biashara bila mtaji


Wengi huamini kuwa lazima uwe na fedha ndiyo uanzishe biashara na ndiyo sababu yao kuu ya kukaa bila kujishughulisha. Ukweli ni kwamba mtaji ni moja ya kitu muhimu katika kuanzisha biashara, lakini kuna aina ya biashara ambazo zinahitaji gharama ndogo kuanzisha na kukupelekea kupata faida kubwa.

Kama mfanyabiashara unaweza kutoka kwa kishindo kwa kuanza ukiwa huna kitu na kufanya kazi kwa juhudi ukiwa upande wa huduma na kufanikiwa kutengeneza faida kubwa na kutokea hapo na kuanza kufikiria kuanza kukodi ofisi yako, kuajiri watu wengine na kadhalika.

Ingawa ni rahisi kutoka ukiwa upande wa huduma lakini inahitaji ujuzi au weledi fulani hivi ili uweze kufika kilele cha mafanikio. Hapa simaanishi lazima uwe umesoma chuo kikuu maana ujuzi au utaalamu wa jambo halihusiani na digrii ya chuo kikuu.

Unaweza pata ujuzi kwa kuhudhuria semina na warsha mbalimbali au kufundishwa na mtu mwenye ujuzi husika na baada ya kupata ujuzi kuanza kuufanyia kazi katika maisha yako ya kawaida kila siku na kuwa bora kwa upande huo.

Nimejaribu kuorodhesha aina zaidi ya 14 unazoweza kuanzisha pasipo kuwa na mtaji kabisa au mtaji kidogo sana. Hizi ni aina ya biashara ambazo nimezifanya kwa muda sasa na kuona matunda yake na nyingine nimeshuhudia watu wakifanya na kufanikiwa.

Kama kweli una shauku ya kweli kuanza leo biashara soma kwa umakini sana na kuona je, ni wapi pa kuanzia ili uweze kutimiza lengo lako la maisha.

Zifuatazo ni baadhi ya biashara unazoweza kuanzisha kwa mtaji mdogo au pasipo mtaji kabisa. Hizi ni kama vile huduma za kuandika miradi biashara, mshauri wa mambo ya biashara, huduma za kuandaa vitabu vya hesabu, kutoa huduma ya kuandaa nakuendesha matukio, kuanzisha tovuti kwa huduma mbalimbali, mshauri wa masoko, mtafasiri wa maandiko mbalimbali kwenda lugha ya wazawa, kutafiti fursa mpya za biashara, kutoa huduma za kuchapisha, kutoa huduma za kuajiri, mshauri wa mitandao ya kijamii na kutoa huduma za kuandikisha majina ya kampuni.

Ukweli ni kuwa wajasiriamali wengi hawajui hata kuandika ‘business plan’ katika uwezo wa kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza na huwa hawawekezi muda wa kutosha kujifunza kwa hilo. Kama unaweza timiza hitaji hili biashara ipo mikononi kwako.

Mshauri wa mambo ya biashara: Wewe ni una uzoefu wa ujasiriamali au umiliki wa biashara? Unajua nini kinahitajika ili uanzishe biashara, kujenga biashara, kuongeza biashara na kukua? Sasa unaweza kuanza kazi ya ushauri wa biashara. Unaweza kusaidia kampuni au biashara mbalimbali kutoka chini ya uvungu na kwa kutoa ushauri na maelekezo muhimu. Unaweza kuwasaidia watu walioajiriwa kuanza kutoka kwenye ajira na kuingia kwa ujasiriamali kwa malipo.

Huduma za kuandaa vitabu vya mahesabu. Wewe ni mzuri katika kuandaa vitabu vya uhasibu vya kampuni au biashara mbalimbali? Unaweza kuweka ulingano kwa vitabu vya uhasibu. (Hili ni jambo huwa na shauku kulipata). Sasa hamna kitu kinaweza kukuzuia wewe kuanza huduma za kuandaa vitabu vya mahesabu. Anza sasa.

Kutoa huduma ya kuandaa na kuendesha matukio (Event management), kampuni nyingi kila mara huwa na matukio mbalimbali mfano semina, siku ya familia, sherehe mbalimbali. Mara nyingi kampuni kama kampuni haiwezi kufanikisha kwa ufanisi uandaaji wa matukio haya na hivi ndivyo ilivyo kutokana na wafanya kazi wao kuwa na majukumu.

Hivyo ili kuwa na ufanisi hapa inabidi kampuni zikodi watu wanye ujuzi wa kuandaa shughuli husika kwa uhakika. Wewe kama una ujuzi na uzoefu wa kuandaa shughuli kama hizo; mwanzo mpaka mwisho, uwanja ni wako. Mfano kuna matukio kama siku ya familia, semina kwa wafanyakazi, maonyesho ya biashara ndani na nje ya nchi.

Kuanzisha tovuti kwa huduma mbalimbali. Kwa Afrika watu kunufaika na tovuti ndio kwanza ipo hatua za mwanzoni. Unaweza kuanzisha tovuti na kutoa huduma ya taarifa. Watu wengi wanaotembelea tovuti yako wanaweza kuongea na kampuni kadhaa kuja kutangaza na wewe na kutengeneza fedha za kutosha.

Kama hujui jinsi ya kutengeneza tovuti usijali kuna tovuti za bure kabisa ambazo zimetengenezwa tayari kinachohitajika ni wewe kujaza fomu zao na ndani ya dakika moja unakuwa na wewe tovuti yako na kama unahitaji nunua domain, unaweza ukawa moja kwa moja tovuti yako. Tovuti unazoweza ingia na kutengeneza tovuti yako bure ni www.weebly.com,www.webs.com au pia unaweza tengeneza blog ikawa unaweka taarifa watu wanatafuta na kisha kutafuta wadhamini wa hiyo blog.

Mshauri wa masoko. Je wewe unaweza ukanionyesha njia ya gharama ndogo ya kuongeza wateja kuanzia asilimia 30 hadi 70 au zaidi? Kama ndio biashara ipo mikononi mwako. Unaweza ukajiweka wewe mwenyewe katika ushauri wa masoko kwa wamiliki biashara ndogo na kati hata kubwa jinsi ya kuteka na kuwavuta wateja na kuongeza mauzo ya bidhaa kwa ada fulani, kutokana huduma husika.

Mtafasiri wa maandiko mbalimbali kwenda lugha ya wazawa; Kampuni nyingi za nje zinazokuja hapa nchini, huwa wanahitaji kutafsiri taarifa zao kwenda lugha ya wazawa, mfano mradi fulani, tovuti zao, mfano kama ni kampuni ya vitabu mwandishi mmiliki angependa ili auze kwa wazawa inabidi atafasiri kwenda lugha ya wazawa. Mfano kuna hata miradi mbalimbali ambayo inatakiwa iangaliwe na wazawa.

Kutafiti fursa mpya za biashara: Nina marafiki zangu ambao walianza kutoa huduma ya kutafiti fursa mpya na wanafanya vyema kwenye hii biashara. Wanachofanya kutupia jicho kwa mambo yajayo, mwelekeo, mahitaji aua fursa za biashara na kuandaa mradi au mpango kuhusiana hilo na kuuza hilo wazo kwa kampuni makubwa.

Kutoa huduma za kuchapisha. Biashara hii inafahamika na wengi lakini bado inalipa. Unaweza kuanza kutoa huduma ya kuchapisha business, banner sposters card, viperushi na catalogues kwa biashara ndogo na za kati.

Kutoa huduma za kuajiri. Siku hizi kazi za managementi za rasilimali watu kwa kampuni nyingi hutolewa na tenda kwa kampuni za nje ya kampuni husika kufanya hiyo kazi ili kuongeza ufanisi kwa kampuni husika na hivyo kupelekea kampuni husika kuweka umakini wake wa kutimiza lengo lake mahususi.

Kama una uelewa na ujuzi wa kutosha wa kushughulika na maswala ya rasiliamali watu uwanja ni wako. Kwa sasa hapa Tanzania kujisajili kuwa wakala wa kuajiri ni bure unatakiwa uende pale wizara ya ajira na vijana kujisajili.

Mshauri wa mitandao ya kijamii (social media consultancy). Kwa hii dunia mitandao ya kijamii imechukua asilimia kubwa. Je wewe unajua jinsi ya kutengeneza foleni kwa mitandao ya kijamii? Unajua jinsi ya kuboresha na kuelimisha umma juu ya chapa (brand) za makampuni ndani ya mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na linked in? Basi unaweza kuwa mashauri wa mitandao ya kijamii na kutengeneza fedha zako.
Kutoa huduma za kuandikisha majina ya kampuni. Je wewe ni mzuri katika kuandika katiba za kampuni? Unajua jinsi ya kuchagua jina sahihi la kampuni? Unajua hatua zinazohitajika ili ukamilishe uandikishe jina la biashara? Anza sasa fungua biashara yako ya kutoa huduma za kuandikisha majina ya kampuni.

Huduma nyingine unazoweza kuzifanya ili kutengeneza fedha ni kutoa huduma za kuandikisha haki mili za bidhaa au huduma huduma za ushauri kwa biashara ndogo au kuandika vitabu vya uelimishaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni